Kundi la Ze Comedy lililojipatia umaarufu nchini kwa maigizo yao, jana lilikuwa miongoni mwa wageni waliofika kujionea vikao vya Bunge vinavyoendeshwa mjini hapa. Wasanii hao walitambulishwa kwa wabunge baada ya kipindi cha maswali na majibu asubuhi. Naibu Spika Anne Makinda, wakati akiwatambulisha wageni hao aliosema ni maalumu, alisema wamefika hapo kwa mwaliko wa wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam. Wabunge walipiga makofi wakati wa utambulisho huo ambao awali Naibu Spika hakutaja majina yao, hadi mbunge mmoja alipotaja kuwa ni Ze Comedy, ndipo akawataja kwa majina. Wasanii waliotinga ndani ya Bunge hilo ni pamoja na kiongozi wao, Emmanuel Mgaya ‘Masanja’, Lucas Mhuville ‘Joti’, Sekioni David ‘Seki’, Mujuni Sylivery 'Mpoki', Isaya Mwakila ‘Wakuvanga’. Wakati wakitambulishwa wakiwa ndani ya suti za Kimagharibi, baadhi yao walivaa miwani ambayo imekuwa ikiwatambulisha wakati wanapofanya maigizo yao kwenye televisheni. Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Wakuvanga alisema wamekuja bungeni kwa nia ya kujifunza jinsi chombo hicho cha kutunga sheria kinachofanya kazi zake. Alisema walichojifunza ni kwamba baadhi ya viti vya wabunge vinakosa wabunge; wabunge wanafikiria kwa kufumba macho na wakati mwingine hutaniana.Wabunge walifurahi sana, pia walijumuika nao katika chakula cha mchana.Source: Habari leo
No comments:
Post a Comment