MAKANISA YANAVYOBOMOA NDOA ZETU

Na Anti Flora


Mpenzi msomaji, makanisa mengine hasa yanayojiita ya walokole, ni kichekesho kitupu. Ingawa waumini wake hujiunga kutokana na imani zao, lakini mwisho wa siku wengine hujikuta matatani. Hebu sikia mifano hii mitatu iliyo hai uweze kutafakari jinsi baadhi ya makanisa yalivyochipuka kama uyoga yanavyochangia hofu, mitafaruku ndani ya familia zetu. Utadhani ni ndoto kumbe ni kweli yametokea. Nianze na mfano mmoja uliotokea wiki iliyopita pale eneo la Kimara Stopover jijini Dar es Salaam. Wapo ndugu zangu wawili walioshuhudia tukio hilo, kisha wakanisimulia nikashawishika kuwamegea wasomaji wangu leo. Ndugu zangu hawa (mabinti) wanasimulia hivi; Wakiwa wanapita kuelekea dukani walimwona mama mmoja akiwa amembeba mtoto mdogo, huku akiwa amesimama na baba mmoja aliyepiga tai nje ya kanisa moja la walokole. Ilikuwa majira ya saa mbili hivi usiku. Ndani ya kanisa hilo kulikuwa giza lakini ilikuwepo minong\'ono ya watu. Robo saa baadaye, mabinti wale wakiwa wanarejea, wakawa wanaongozana na baba mmoja aliyekuwa amefunga POP mkono wa kushoto kuashiria alikuwa ameumia mfupa wa mkono. Baba huyu alikuwa akizungumza na simu ya kiganjani kwa hasira akitoa matusi mazito. Baadhi ya maneno yalikuwa; ``uko wapi mshenzi we, usiniambie uko kanisani hadi muda huu saa mbili, hawajui una mume? Una mtoto mdogo, utanipikia saa ngapi? ``Hilo ni kanisa gani kama siyo matapeli, au wanakutaka hao wachungaji wako niwakabidhi, nitafute mwingine? Baba huyu alitoa maneno mfululizo na alipokaribia usawa wa kanisa lile akamuona mkewe akiwa amesimama na bwana yule (inadaiwa ni mchungaji). Kumbe awali mama mtoto alimdanganya mumewe eti ameshatoka anakaribia nyumbani, kumbe bado yuko kanisani. Ghafla mama akashtukia baba anamdaka kwa mkono mmoja. ``Hapa ndio nyumbani, kwa nini unanidanganya... huyu ndio mchungaji anayekudanganya usiwahi nyumbani (wakati huo akamshika mke na kumnyang\'anya ile simu huku akimpiga makofi. Yule mchungaji kuona ngoma nzito akakimbilia kanisani na punde akatoka na wenzake wawili. Sasa wakaanza kumsihi bwana yule aache shari kisha waelewane. Bwana huyu akawa mbogo na kuanza kuondoka. Baada ya hatua chache akarejea pale na kung`aka, ``leta funguo za nyumba``, alimwambia mkewe. Huku mke akijaribu kukataa, yeye akazitwaa kwa nguvu na kuishia zake huku akimwacha mke na wachungaji wake. Mpenzi msomaji, unaonaje kisa hiki Kituko hiki kinanikumbusha tukio moja kule Moshi mkoani Kilimanjaro eneo la Kiboriloni, Msaranga mwaka mmoja hivi uliopita. Lipo kanisa moja lilizua mtafaruku hata kufikia hatua ya kuchomwa moto, (Ilikuwaje? Kanisa hilo inasemekana waumini wake upo wakati wanavua nguo zote na kusali usiku. Yupo baba mmoja ambaye mkewe alikuwa muumini. Baba huyu aliposimuliwa kuwa waumini huvua nguo zote na kubaki uchi akashtuka hivyo kuweka mtego. Alichofanya ni kuvizia siku hiyo ya kusali uchi akaenda na kujificha. Ulipofika muda wa kuvua nguo waumini wote wakafanya hivyo, na baada ya muda wote wakawa kimya. Ndipo baba huyu akajitosa ndani huku akipiga kelele ya kumtaka mkewe arudi nyumbani. Waumini kusikia vile wakaanza kutimka kila mtu kivyake wakiwa watupu. Hakika ilikuwa patashika nguo chanika. Tokea siku ile baba huyu akaungana na wenzake ambapo siku moja walilimwagia petroli kanisa hilo na kulichoma moto, kisa linavunja ndoa zao. Swali ni je, waumini mchanganyiko (wanaume na wanawake) kuvua nguo eneo moja, usalama wao kimapenzi uko wapi? Yaani mbuzi umwekee majani aache kuyala? Hebu tuache utani makanisa mengine hayajengi bali yanabomoa nyumba zetu. Huo ndio ukweli. Kisa kingine kinamhusu wifi yangu mmoja. Yeye na familia yake ni waumini wa kanisa katoliki ndani ya ubatizo. Lakini wifi huyu miaka michache iliyopita akageukia kanisa moja la walokole huko Mabibo Dar es Salaam ambako alimshawishi pia mumewe na watoto wao watatu. Nilipowadadisi nikagundua kuwa eti kanisa hili huwapa nauli ya kwenda na kurudi waumini wake hasa wasio na uwezo. Sisi kama familia tukawa tunajiuliza; kanisa katoliki liko karibu na tunapoishi, unatembea kwamiguu. Lakini kule mabibi lazima upande mabasi mawili kwenda na kurudi. Tukajiuliza, kanisa hili linalipia nauli waumini wangapi? Bado tunahisi lipo jambo lililojificha kati ya mama huyu (wifi) na hao wachungaji wake Mungju anisamehe lakini mashaka kwa mwanadamu lazima yawepo. Wapo waumini wengi wamehama makanisa yao ya awali na kujiunga na yale ya ulokole. Lakini baadhi wamejikuta katika mitafaruku mikubwa ikiwa ni pamoja na kuvunjika ndoa takatifu au kutengana. Kisa imani ya kusaka wokovu. Kusaka wokovu ni jambo muhimu katika maisha haya. Lakini kwa namna gani wokovu huu unasakwa ndio kitendawili kilichopomikononi mwetu. Kama wanaosaka wokovu huu wanadanganyika ndio hao hao wanaoumbuka hadharani. Ni muhimu kila muumini awe makini na kanisa mengine yamechipuka kama uyoga kusasa waumini kwa gharma zote, kumbe ni wavurugaji tu. Kama wazazi wako wamekubatiza kwa dini zao, iweje leo uwageuke na kujiunga na dini ambazo nyingine ni matatizo makubwa makanisa mengine hawaamini msalaba, mtu akizikwa ni kaburi kujaa udongo kisha basi. Sisemi watu wasijiunge na makanisa hayo lakini ni vema wakayapima kwanza ili wasijikute kwenye mitafaruku kama niliyotolea mfano hapo juu. Mpenzi msomaji, mimi nakomea hapa kama nawe unalo la kuchangia unakaribishwa. Nikandamizie kupita email; fwingia@yahoo.com Wasalaam.
SOURCE: Nipashe

No comments: